Tuesday, February 12, 2013

Nigeria mabingwa Afcon 2013

Wachezaji wa Nigeria wakishangilia ubingwa wao.


Mwananchi, Jumatatu,Februari11  2013

NIGERIA ilitawala mchezo wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na kuifunga Burkina Faso bao 1-0 na kutwaa taji mjini, Johannesburg, Afrika Kusini.
Sunday Mba alikuwa shujaa wa ushindi wa Nigeria (Super Eagles) baada ya kufunga bao pekee dakika tano kabla ya filimbi ya kutenganisha nusu ya mchezo huo mkali ulioshuhudiwa na watazamaji 85,000.
Wilfried Sanou angeweza kusawazisha bao hilo kwa Burkina Faso (Stallions) katikati ya kipindi cha pili, shukrani kwa kipa wa Nigeria Vincent Enyeama aliyecheza vizuri kuokoa hatari hiyo.
Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Nigeria hatua ya fainali tangu mwaka 2000, na walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa taji mbele ya Burkina Faso, taifa dogo Afrika Magharibi.
Burkina Faso haijawahi kuifunga Nigeria katika mechi 12 walizokutana katika mashindano mbalimbali, na hiyo ilitosha kuipa Nigeria nafasi ya kushinda mchezo. Efe Ambrose alikuwa na nafasi tano za kufunga kipindi cha kwanza, lakini ya kukumbukwa zaidi ni pale alipopiga juu mpira akimalizia kiki ya adhabu ndogo kutoka kwa Victor Moses ndani ya dakika saba tangu kuanza mchezo.
Nigeria waliotawala mchezo kwa kiasi kikubwa, walikaribia kufungwa kama siyo, Aristide Bance kupoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya shuti lake la mita 25 kukosea shabaha na kwenda nje ya lango huku.
Nigeria wangeweza kufunga bao la pili kama Ideye angetumia vizuri pasi aliyopewa kuusindikiza kirahisi mpira wavuni, lakini akaishia kupiga nje.
Huo ni ubingwa wa tatu kwa Nigeria, lakini wa kwanza kwa tangu mwaka 1994 walipotwaa mara ya mwisho baada ya kuifunga Zambia mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.


REKODI
Nigeria:
Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi anakuwa kocha wa pili kama mchezaji kutwaa taji na pia kama kocha katika historia ya michuano hiyo, akiungana na Mahmoud Al Gohari wa Misri.
Nigeria ina rekodi ya pekee ya kiwango cha ubora wa soka duniani (Fifa), kwani ndiyo timu pekee Afrika iliyowahi kushika nafasi ya tano duniani mwaka 1994. Kwa sasa inashika nafasi ya 52.Kwa mara ya kwanza Nigeria ilicheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994, ikiwa kundi moja na Bulgaria, Ugiriki na Argentina na kufanikiwa kuongoza kundi lake.
Iliifunga Bulgaria 3ñ0, ikapoteza kwa kufungwa mabao 2-1 na Argentina na kufanikiwa kusonga mbele raundi ya pili baada ya kuifunga Ugiriki mabao 2ñ0.
Katika raundi ya pili, Nigeria ilicheza na Italia, ambapo mpaka dakika 25 za kwanza tayari walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Amunike.
Burkina Faso:
Kwa upande wa Burkana Faso, haina rekodi nyingi na nzuri za mafanikio katika soka la kimataifa kama ilivyo kwa Nigeria. Awali, Burkina Faso ilikuwa ikijulikana kama Upper Volta mpaka mwaka 1984, ilipobadilika jina na kuwa la sasa. Waliandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1998 na kumaliza katika nafasi ya nne, lakini mafanikio makubwa waliyopata ni kufika hatua ya fainali mwaka huu.

No comments:

Post a Comment